TAMKO TOKAA TCRA(MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA)

Habari Leo 11 August 2015
Meneja Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy akiwaeleza waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusu matumizi mabaya ya mitandao.

MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kiama kwa watumiaji vibaya na wahalifu wote wa mitandao nchini, kuwa siku zao zinahesabika kwani ifikapo Septemba mosi, mwaka huu, Sheria ya Uhalifu wa Mitandao itaanza kutumika na wengi huenda wakaishia gerezani.

Mamlaka hiyo imebainisha kuwa kwa sasa Tanzania inaongoza kwa kuwa na watumiaji vibaya wengi wa mitandao ya kijamii, jambo linalosababisha taarifa za mitandao mingi kutoaminika hadi nchi za nje kutokana na kujaa uzushi, uongo, uchochezi na lugha na picha za matusi.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy alikiri kuwa pamoja na kwamba mamlaka hiyo imefanya kazi kubwa ya kuelimisha jamii juu ya utumiaji sahihi wa mitandao hiyo, bado matumizi yake si mazuri hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi na kwa watu maarufu.

“Napenda kuwatahadharisha Watanzania na watumiaji wa mitandao hii kwa ujumla kuwa sheria hii si ya kupuuzwa, kwani kwa hali ilivyo wengi watatozwa faini na watashindwa kulipa na kuishia gerezani,” alisisitiza.

Alisema kutokana na kukithiri kwa matumizi mabaya ya mitandao nchini, kwa sasa nchi nyingi haziamini tena taarifa za mitandao ya kijamii na wala hawazitumii hali inayopaswa kubadilishwa.

“TCRA tumebaini kuwa watu wengi wanatumia mitandao hii lakini hawajui hasa matumizi yake sahihi, tunashauri kabla mtu hajafungua mtandao wake kama vile blogu, ukurasa wa facebook au hata whatsApp lazima wajielimishe kwanza kuwa wanafungua kwa malengo gani, na wataitumiaji kwa manufaa yao na si vinginevyo,” alisisitiza Mungy.

Alisema mamlaka hiyo kazi yake kubwa ni kusimamia matumizi ya mitandao hivyo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola, itahakikisha inadhibiti kwa kuelimisha na kuwabaini wale wote wanaotumia vibaya mitandao hiyo.

“Kazi yetu sisi si kuwakamata hawa wahalifu, sisi tunasimamia na tuna uwezo wa kuwatambua wale wote wanaotumia vibaya mitandao hii hata kama watabadilisha kadi zao za simu mara 300 na kubadili majina, tuna uwezo wa kuwatambua na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria pale tunapotakiwa kwa mujibu wa taratibu,” alisisitiza.

Alisema tayari wameshaanza kampeni ya kuelimisha matumizi sahihi ya mitandao kupitia vipindi na semina zinazojumuisha kada mbalimbali muhimu kama vile wasanii na vyombo vya habari juu ya kujihadhari na matumizi mabaya ya mitandao.

“Hivi karibuni tulifanya semina ya wasanii ambao ndio waathirika wakubwa wa matumizi haya ya mitandao na kuwaelimisha namna ya kuitumia mitandao hii, pia vyombo vya habari tumevielimisha na kuvisisitiza kutotegemea taarifa za mitandao hasa kipindi hiki cha uchaguzi kwa kuwa nyingi si sahihi,” alisema bosi huyo wa TCRA.

Tayari Rais Jakaya Kikwete ameshasaini Sheria hiyo ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na inatarajiwa kuanza kufanya kazi rasmi Septemba mosi, mwaka huu. Sheria hiyo katika eneo la adhabu kwa wahalifu wa mtandao pamoja na wasambazaji wa picha za utupu na ngono, wasambazaji wa taarifa za uongo, za kibaguzi na matusi na watu wengine wanaofanya udanganyifu unaohusu kompyuta, adhabu ni kwenda jela hadi miaka 10 au kulipa faini isiyopungua Sh milioni 50.

Kwa upande wa kusambaza picha za ngono, matusi, uasherati atalipa faini isiyopungua Sh milioni 30 au kwenda jela miaka 10 au vyote. Lakini mtu atakayesambaza picha za utupu atalipa faini isiyopungua Sh milioni 20 au kwenda jela miaka saba au kutumikia adhabu zote kwa pamoja.

Pia kwenye muswada huo mtu ambaye atatoa taarifa, takwimu au maelezo kwa njia ya picha, maandishi, alama au aina nyingine yoyote zikiwa ni za uongo akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua Sh milioni tatu au kutumikia kifungo jela kisichopungua miezi sita au vyote.

Kwa upande wao, Jeshi la Polisi Tanzania, limesema tayari limeanza kuchukua hatua dhidi ya watumiaji vibaya wa mitandao ya kijamii na hadi sasa imekamata watumiaji hao wengi na wako katika hatua ya kuhojiwa na wengine kufikishwa mahakamani.

“Natumia fursa hii kuwaonya watu waache tabia ya kutengeneza ujumbe wa uchochezi, matusi, uongo na uzushi kwa visingizio vya itikadi, dini na siasa kwani Jeshi la Polisi halitovumilia tabia hizo na watakaobainika watafikishwa kwenye vyombo vya sheria,” alisema msemaji wa jeshi hilo, Advera Bulimba.

Alikiri kuwapo na tabia ya watu kuandika kwenye mitandao ya kijamii taarifa za uchochezi na uzushi dhidi ya watu maarufu wakiwemo viongozi au taasisi na baadhi yao wanachunguzwa na wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria.

Alitolea mfano wa mmoja wa watumiaji mtandao ambao jeshi hilo lilibaini aliandika taarifa za uchochezi kuhusu tukio la ujambazi na mauaji la Kituo cha Stakishari Ukonga jijini Dar es Salaam na sasa anakabiliwa na kesi ya uchochezi mahakamani.

Comments

Popular posts from this blog

STORY YA KUSISIMUA

FORM FIVE SELECTION 2016 CHECK HERE

CHOMBEZO FUPI INAITWA ««JAMANI ANKO»» ISOME HAPA